KASRI 2
"Hapana Albert, ukiondoka kila kitu kitajulikana......naweza kunyongwa kwa kosa la kumdanganya mfalme kwa miaka yote hiyo....." Helena alisimama akimsihi Albert asiondoke huku akiwa ameushika mkono wake.....
Kimya kilitawala kidogo ambapo Albert na Helena walisikia kama nguo ikikwaruza ukuta, ilikuwa ni kama mtu aliyejibanza na ukuta akijaribu kusogea mbali baada ya kusikiliza mazungumzo yale. Albert alizunguka nyuma ya ukuta ule kulipokuwa na chumba cha stoo kisha akamdaka mtu aliyekuwa kwenye harakati za kunyata ili aondoke eneo lile.
“ Tulia hapo, we ni nani....".Albert alimuuliza na kabla hajapewa jibu alimtambua mtu yule kwamba ni James, mtoto wa mke wa kwanza wa mfalme. Albert aliuachia mkono wa James huku akishangaa kwa hofu akijua kwamba siri kubwa imejulikana... “ Wewe umefata nini hapa, umesikia kitu gani.. "
James bila kuzungumza chochote aliondoka akimkata Albert jicho kali. Albert aligeuka na kumfuata Helen ambaye kwa wakati huo alikuwa amejibanza ukutani kwa woga akiwasikiliza.
“James amefahamu, ni lazima amwambie Mama yake. Tutafanyaje? " Albert aliuliza akimtazama mama yake bila kupepesa jicho.
Helena alikimbia chumbani kwake akilia bila kuzungumza jambo lolote.........
Albert alirudisha kumbukumbu zake baada ya mlinzi kumuamuru atoke kule ndani.
*******
Mfalme aliandaa karamu fupi ya kuwaalika marafiki zake kutoka falme jirani.
Meza zilipambwa vizuri, wake kwa waume wakivaa mavazi mazuri na ya kupendeza. Vyakula vingi vya kila aina viliiandaliwa pamoja na vinywaji vilivyotengenezwa kwa umakini haswaa.
Wageni waliingia na kukaribishwa na Mfalme Duncan. Wake zao pia walipokelewa kwa shangwe na wake za Mfalme. Mabinti wao, warembo na wenye kupendeza waliungana na mabinti wengine wa Haven kucheza na kudansi.
Baada ya kupata chakula Mfalme aliazimia kutoa utambulisho mfupi ili familia za kigeni ziitambue familia yake. Alianza kwa kumtambulisha Charlotte kisha Victoria. Mfalme alijaribu kumtafuta Helen katika meza ile kubwa na kutambua kwamba kwa siku hiyo Heleni hakujitokeza katika hafla ile.
“Mke wangu mwingine naona atakuwa anafanya jambo fulani mda sio mrefu atakuwepo.....ngoja tuendelee kuwatambulisha watoto....."
Mfalme alitoa utambulisho lakini pia aligundua kwamba Albert hakuhudhuria hafla ile. Mfalme alikasirika sana....
Baada ya ugeni ule kuondoka, mfalme aliamuru Helen na Albert watafutwe na wapelekwe mbele yake.
Walipofika mbele ya mfalme, walikuwa wameelekeza macho yao chini...
“Mke wangu mwaminifu ambaye hujawahi kuniangusha, una tatizo?" Mfalme aliuliza kwa upole kisha akasimama.
“Uliona ni vyema usihudhurie hafla hii muhimu ili niaibike?"
Mfalme aliuliza maswali yasiyotaka majibu kisha akamgeukia Albert,
“Wewe na mama yako mna shida gani. Kwanini hamkuhudhuria hafla......"
“Samahani baba......." Albert aliongea akitazama chini.
“Hiyo inaonesha jinsi gani mwana anamheshimu mama yake kuliko baba. Wote wameshauriana kukuvunjia heshima leo......" James aliyetokea kwenye lango kubwa la dhahabu alizungumza huku akimsogelea Charlote ambapo wote walikaa wakitazama tukio lile.
Mfalme aliposikia maneno yale aliinama chini kisha akainua uso uliokuwa na ghadhabu kubwa......

Comments